poesia swahili [kezilahabi_kithaka wa mberia_alamin mazrui]

Upload: unfo

Post on 17-Feb-2018

258 views

Category:

Documents


0 download

TRANSCRIPT

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    1/20

    http://www.poetrytranslation.org

    POESIA SWAHILI

    EUPHRASE KEZILAHABI

    KITHAKA wa MBERIAALAMIN MAZRUI

    http://www.poetrytranslation.org/http://www.poetrytranslation.org/
  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    2/20

    INDICE

    EUPHRASE KEZILAHABI3 Upepo wa Wakati4 Mafuriko5 Mgomba6 Chai ya Jioni

    7 Fasihi8 Kisima

    KITHAKA wa MBERIA9 Jumapili ya Damu

    ALAMIN MAZRUI12 Mlango13 Mimi Ni Mimi14 Nilivuka15 Kifungoni16 Kizuizini17 Bega kwa bega18 Sauti?

    19 Mkata wa maneno20 Niguse

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    3/20

    EUPHRASE KEZILAHABI

    Upepo wa WakatiJuu ya mlima mdogo

    Siku moja nilisimama.

    Nikatazama chini ziwani, siku

    Ya dhoruba. Halafu niliona mawimbi

    Yakipanda na kushuka. Yakivimba,

    Yakiviringika, yakigongana na kutoa povu

    Kama fahari wehu katika bonde lisomajani.

    Yalivyotengenezwa!

    Yalivyofifia na kuanza tena!

    Kamwe sikuona.

    Lakini niliyaona yakishuka kwa nguvu

    Na kupanda haraka, yakisukumwa

    Na upepo wa Magharibi na Mashariki.

    Hivyo ndivyo ulimwengu ulivyo.Na hivyo maisha ya binadamu.

    Wanapanda na kushuka

    Wakisukumwa na upepo na wakati.

    Tazama wanavyojinyakulia madaraka

    Kama mzamaji, mguu wa rafikiye, ashikavyo!

    Wanavyoshika pesa kama mtoto

    Na picha ya bandia

    Au asikari mwehu na bunduki yake

    Na kutunyamazisha!Watapanda na kushuka

    Na wataanguka kweli!

    Wakisukumwa na upepo wa wakati!

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    4/20

    MafurikoNitaandika wimbo juu ya mbawa za nzi

    Utoe muziki arukapo wausikie walio wengi

    Ushairi wa jalalani utaimbwa

    Juu ya vidonda vya wakulima

    Na usaha ulio jasho lao.

    Nitaandika juu ya mbawa za wadudu

    Wote warukao

    Juu ya mistari ya pundamilia

    Na masikio makubwa ya tembo.

    Juu ya kuta vyooni, maofisini, madarasani,

    Juu ya paa za nyumba, kuta za Ikulu,

    Na juu ya khanga na tisheti.Nitaandika wimbo huu:

    Mafuriko ya mwaka huu

    Yatishia nyumba kongwe bondeni.

    Waliomo wameanza kuihama

    Na miti ya umeme imeanguka.

    Palipokuwa na mwanga, sasa giza.

    Mafuriko ya mwaka huu!

    Mti mkongwe umelalia upande

    Wa nyumba zetu hafifu.Upepo mkali uvumapo hatulali.

    Kila kukicha twatazama mizizi yake

    Na mkao wake, na kuta hafifu za nyumba.

    Lazima ukatwe kuanzia matawi hadi shina

    Mafuriko ya mwaka huu yaashiria...

    Tutabaki kuwasimulia wajukuu:

    Mwaka ule wa mafuriko

    Miti mingi mikongwe ilianguka.

    Mafuriko ya mwaka huu!Wengi wataumbuka.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    5/20

    MgombaMgomba umelala chini: hauna faida tena,

    Baada ya kukatwa na wafanya kazi

    Wa bustani kwa kusita.

    Watoto, kwa wasiwasi wanasubiri wakati wao

    Bustanini hakuna kitu

    Isipokuwa upepo fulani wenye huzuni,

    Unaotikisa majani na kutoa sauti ya kilio.

    Hivyo ndivyo ufalme wa mitara ulivyo.

    Mti wa mji umelala chini: hauna faida tena,

    Baada ya kukatwa na wafanya kazi

    Wa bustani kwa kusita.

    Chumbani hakuna kituIsipokuwa upepo fulani wenye huzuni utingishao

    Wenye hila waliokizunguka kitanda na kulia.

    Machozi yenye matumaini yapiga

    Mbiu ya hatari ya magomvi nyumbani.

    Magomvi

    Kati ya wanawake

    Magomvi

    Kati ya watoto kwa ajili ya vitu na uongozi.

    Ole! Milki ya 'Lexanda imekwisha!

    Vidonda vya ukoma visofunikwa

    Ambavyo kwa mda mrefu vilifichama

    Sasa viko nje kufyonzwa na inzi wa kila aina

    Na vinanuka vibaya.

    Lakini inzi kila mara hufyonza wakifikiri

    Nani watamwambukiza.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    6/20

    Chai ya JioniWakati tunywapo chai hapa upenuni

    Na kuwatazama watoto wetu

    Wakicheza bembea kwa furaha

    Tujue kamba ya bembea yetu

    Imeshalika na imeanza kuoza

    Na bado kidogo tutaporomoka.

    Kulikuwa na wakati ulinisukuma juu

    Nikaenda zaidi ya nusu duara;

    Kulikuwa na wakati nilikudaka

    Ulipokaribia kuanguka,

    Na kulikuwa na wakati tulibebana kwa zamuMmoja wima akisukuma mwingine amekaa.

    Wakati huo, japo tulipaa mbele na nyuma

    Tulicheka kwa matumaini yaliyotiwa chumvi

    Na kisha tukaongozana jikoni kupika chajio;

    Ilikuwa adhuhuri yetu.

    Sasa tukisubiri ndoto tusizoweza kutekeleza tena

    Tumalizie machicha ya chai yetu ya jioni

    Bila kutematema na kwa tabasamu.Baada ya hapo tujilambelambe utamuutamu

    Uliobakia kwenye midomo yetu,

    Tukikumbuka siku ilee ya kwanza

    Tulipokutana jioni chini ya mwembe

    Tukitafuta tawi zuri gumu

    La kufunga bembea yetu

    Naye mbwa Simba akikusubiri.

    Lakini kabla hatujaondoka kimyakimyaKukamilika nusu duara iliyobakia.

    Tuhakikishe vikombe vyetu ni safi.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    7/20

    FasihiManeno yangu kumeza tena sasa siwezi.

    Lakini kuonyesha ukweli na kuutafuta

    Nitaendelea: mimi ni kama boga.

    Nimepandwa katikati, bustanini,

    Na kama boga nitatambaa chini

    Zote pande, kuikwea miti ya hekima

    Na yote magugu koo kuyakaba.

    Bila woga, bila nyuma kurudi nitashambulia

    Ya binadamu matendo bado yakihema.

    Halafu wakati

    Ujao utafika

    Matunda nitatoa

    Makubwa madogo

    Mazuri mabaya

    Wakati utafika watakapokuja wajuzi

    Kwa jembe la wino kunipalia.

    Wala mboga za majani watanichuma.

    Utafika, wa maboga kuwa mikata.

    Machafu na safi yatachotwa

    Na nitaingia mitungi ya kila mji-shamba.

    Watoto mikononi mwao watanichezea.Chini wataniangusha na kunipasua.

    Lakini mbegu, mbegu zitabaki.

    Mimi ninajua

    Hatari sina

    Wajibu msomaji

    Mjini na shamba

    Vizuri kunichambua.

    Halafu utafika ule wakatiWatumia vikombe dhahabu na glasi

    Pembeni kwa chuki kunitupa,

    Na nitakuwa nyuma ya wakati

    Lakini wakisahau wahenga

    Kata na mboga walitumia

    Msingi wa wao utamaduni

    Watakuwa wameutupa.

    Kumbukeni, kumbukeni, kumbukeni.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    8/20

    KisimaKisima cha maji ya uzima ki wazi

    Na vyura katika bonde la taaluma watuita

    Tujongee kwa mahadhi yao

    Yaongozayo pandikizi la mtu

    Kwa hatua ndefu litembealo

    Na sindano ya shaba kitovuni

    Upinde na mishale mkononi

    Kisha likapiga goti kisimani

    Tayari kumfuma akaribiaye

    Maana shujaa hafi miongoni mwa wezi

    Bali kama simba mawindoni.

    Hatuwezi tena kuteka maji

    Na kalamu zetu zimekauka wino.

    Nani atamsukuma kwa kalamu

    Aitwe shujaa wa uwongo!

    Aliyeitia kitovuni kwa hofu

    Ingawa tegemeo hakulipata

    Alifungua mlango uelekeao

    Katikati ya ujuzi na urazini mpya

    Mwanzo wa kizazi tukionacho.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    9/20

    KITHAKA wa MBERIA

    Jumapili ya DamuI

    Midundo ya Reggae

    Inarindima hewani

    Na kuchanganyika

    Na macheo

    Katika jiji

    Vioo, madirisha

    Na milango

    Inasalimu amri

    Kutoka kumbo kali

    Za wenye njaa

    Na matarajio

    Ya miongo miwili.

    Ndani ya maduka

    Mawimbi ya watu

    Yanapaa, kushuka

    Na kupanda kwingineko

    Huku rafu na kuta

    Zikibadilika sura

    Kama tanzu za miti

    Kiangazi kinapojiri.

    Vifaa vya kila ukoo

    Nguo za kila rangi

    Zinaketi vichwani

    Kuninginia mikononi

    Kulala migongoni

    Au kubanwa kwapani

    Zikibadili makazi

    Na umiliki.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    10/20

    II

    Risasi

    Zinaanza kupiga miluzi

    Na kwa ghadhabu

    Kushtua kutaMilingoti ya stima

    Magari ya rangirangi

    Na nyama na mifupa

    Watu wanaterereka

    Damu inatiririka

    Uhai unaporomoka

    III

    Ghafla

    Midundo ya Reggae

    Inakauka

    Na nyimbo za jana

    Kurudi angani

    Kama uvundo ambao

    Umevamia pua tenaBaada ya kuangushwa

    Na kumbo la upepo

    Kutoka mwangu jikoni

    Barabara ni dhahiri-

    Magari ya rangirangi

    Vifaru vya madoadoa

    Vinatiririka kama mto,

    Bunduki zinalenga kushotoKulia, nyuma na mbele

    Nayo mizinga hatari

    Inatega mbingu;

    Huu mtiririko

    Ni safari ya marejeo

    Anarejea mungu-wa-kinamo

    Kwenye ulingo.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    11/20

    IV

    Katika fahamu

    Mawazo mbalimbali

    Yanapita kwa zamu

    Kama vipepeo na nondoWakipita kwa makundi

    Mbele ya macho;

    Kwa tabasamu

    Nakumbuka Obasanjo

    Na uamuzi wake angavu

    Bali pia

    Kwa huzuni

    Nakumbuka Bokassa na Amin,

    Na Mobutu na Doe,

    Na damu na mafuvu

    Matita ya mafuvu!

    Magurudumu ya mawazo

    Yanafikia njia panda

    Na kwa muda, kukwama

    Kabla ya kuanza safari tena

    Kwenye njia wazi

    Ya serikali ya kiraiaHata inapoongozwa

    Na genge la mazimwi

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    12/20

    ALAMIN MAZRUIAlamin Mazrui

    MlangoAma utapitakatika mlango huu

    au hutapita.

    Ukipita

    kuna hatari

    ya jinalo kulisahau.

    Hayo ni matata

    Mambo hukutizama mara mbili mbili

    Nawe sharuti utazame kando

    uwache yatendeke.

    Usitafute vita.

    Usipopita

    Huenda ukakuta

    maisha mema ya kufuata

    ukahifadhi mawazo yako

    ukaendelea na kazi yako

    ukafa kishujaa nchini mwako

    lakini mengi huenda yakakupita

    mengi yakakupofua, upofu ukakupata

    kwa gharama gani? Sijui.

    Mlango wenyewe

    haumuahidi mtu kitu

    Ni mlango tu!

    http://www.poetrytranslation.org/poets/alamin-mazruihttp://www.poetrytranslation.org/poets/alamin-mazrui
  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    13/20

    Mimi Ni MimiWaniita mkomunisti

    Waniita mkapitalisti

    Waniita mnashinalisti

    Na mimi ni binadamu tu,

    Kwani hilo halitoshi?

    Nchi zinajiwakia

    Mamama wakiomboleza, wakilia

    Tumbi ya watoto wakiumia

    na maneno yote tunayotumia

    kuuana na kuangamia

    Ewe mto

    Tumesimama pambizoni mwako

    machozi yakitudondoka

    yakichanganyika moyoni mwako.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    14/20

    NilivukaNimevuka mabara kuja Afrika

    Lakini siku katu haikufika

    ya milima kuwa vilima

    ya mito kuwa vijito

    vya kuweza kudakiika.

    Sijakufikia mpenzi

    kama kwamba u nyota ya mbali

    kama kwamba umemea baina yetu

    ukuta wa usingizi.

    Nikikushika, mikono huwa haishiki

    ila maiti ilokufa bila haki

    kama kukumbatia damu yangu jiweni

    katika nyumba iloghariki kwa tufani

    ambayo usiku wake umesimama makini

    na asubuhi yake imekwama mbali

    ikisubiri njiani.

    Miaka imenyumbuka baina yetu: damu na moto,

    Daraja nikazikwea zilogeuka ukuta

    Na wewe, ukazama chini baharini

    nisiweze kukugusa.Mashaza yakanichuna, yakikata mishipa

    ya mikono yangu,

    Nami nikaita:

    Ewe Afrika

    mpenzi wa roho yangu,

    mwenzi wa mabuu na giza,

    Nimezunguka miaka mingi kukutafuta

    na safari yangu bado haijakatika

    ewe maiti ulojifinika kwa yako maisha.

    Nimevuka mabara kuja Afrika

    lakini siku katu haikufika

    ya daraja kuweza kuvukika.

    Ewe ulalaye nami kitandani

    U kama nyota ya mbali mbinguni

    ulo milango ilofungwa kwa ndani

    Nami nimesimama nje

    nasubiri baridini.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    15/20

    KifungoniKwa kuangulia juu mbinguni

    na kulia sana kwa matumaini

    samawati imeingia

    mwangu machoni.

    Kwa kuota mahindi mashambani

    na kulia sana kwa mahuzuni

    manjano imeingia

    mwangu machoni.

    Waache majemadari waende vitani

    Wapenzi waende bustanini

    Na waalimu mwao darasani,

    Ama mimi, tasubihi nipeni

    Na kiti cha kale, za zamani

    Niwe vivi nilivyo duniani:

    bawabu mlangoni

    katika kingo ya maumivu ya ndani

    maadamu vitabu, sheria na zote dini

    zitanihakikishia mauti

    nikiwa na njaa au kifungoni.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    16/20

    KizuiziniNikiwa na njaa na matambara mwilini

    nimehudumika kama hayawani

    Kupigwa na kutukanwa

    kimya kama kupita kwa shetani.

    Nafasi ya kupumzika hakuna

    ya kulala hakuna

    ya kuwaza hakuna.

    Basi kwani hili kufanyika.

    Ni kosa gani lilotendeka

    Liloniletea adhabu hii isomalizika?

    Ewe mwewe urukae juu mbinguni

    wajua lililomo mwangu moyoni.Niambie: pale mipunga inapopepea

    ikitema miale ya jua

    Mamaangu bado angali amesimama akinisubiri?

    Je nadhari yake hujitokeza usoni

    ikielekea huku kizuizini?

    Mpenzi mama, nitarudi nyumbani

    Nitarudi kama hata ni kifoni

    Hata kama maiti yangu imekatikakatika

    vipande elfu, elfu kumi

    Nitarudi nyumbani

    Nikipenya kwenye ukuta huu

    nikipitia mwingine kama shetani,

    Nitarudi mpenzi mama ....

    hata kama ni kifoni.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    17/20

    Bega kwa begaBaridi kutoka mlima mwa Kenya inaingia

    Na upepo unavuma, misitu ya Nyandarua ukipasua

    Lakini mimi ni mwanamke wa Kirinyaga

    baridi sitaisikia

    chochote sitakisikia

    isipokuwa sauti ya ardhi yetu

    nchi yetu

    polepole ikinililia.

    Nyumbani...

    kuponda unga kunatusubiri

    kuchuna mboga kunatusubiri

    kuchanja kuni kunatusubiri

    na watoto

    watoto si haba

    nao pia wanatusubiri.

    Lakini kumfuata mume wangu naendelea

    nchi yangu kuipigania

    utu wangu kujirudishia.

    Lala mwanangu lala

    lala unono ukinisubiri.

    Mwezi utakapoinama

    nitarudi, nikulinde nikuamiri

    Juu ya milima

    mwezi umejaa, umechotama

    kwa huruma ukitutazama.

    Njia ni ndefu mno

    Muda ni mfupi mno

    lakini kumfuata mume wangu naendelea

    bega kwa bega nasogea

    utu kuukomboa.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    18/20

    Sauti?Shingo zetu zimechongoka

    asubuhi kuilekea

    lakini usiku wasogea

    ukichimba misingi ya nyumba,

    na ukuta wa dakika nyumba

    kuizunguka.

    Kifo kimeadhimishwa

    na ule wakati uliotandazika

    mpaka

    kila cha zamani kimesahaulika

    isipokuwa majani makavu yalokaukaMitini, mara kwa mara, yakitingisika

    Ati n'nani aliyesikia sauti?

    Kama kwamba kuna mtu huko mbinguni

    wa kutulipia damu yetu iliyomwagwa

    na kumwagika

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    19/20

    Mkata wa manenoZacheka nami zangu chekeo

    zacheka zafurahika

    Sina mawazo

    kichwani leo

    Bado hayajarauka ...

    Nadhani ni asubuhi

    imeanza kuchipuka

    Nayo ndiyo sababu

    ya moyo kuliwazika

    na huu mdundo mtamu

    mwema ulotandazika

    Najichekea ... kwani najua vyema

    kwamba sijazoea hali hii tabasama

    ijitembezayo kwa shairi na kwa ngoma

    ikichezacheza nami ... ikininyegeza kama mke na mume

    kama wapenzi daima

    Najua sijaizoea hali hii ya furaha na shauku

    ijigambayo kwa mchana na usiku

    kufuata mtindo wa manju kila siku

    ... kufuata anasa za dunia

    Ndipo nikawa mkata...

    mkata wa maneno ya furaha na amani

    ya mahaba au dini

    maneno ya kufifisha kisasi cha mja

    juu ya maisha duniani

    maneno ya kushinda vita vya nyoyoni

    hivyo vita vya ndani kwa ndani.

    Neno langu ni maumivu tu, ni mashaka

    Ndipo kapendelea mwenendo wa kale ...

    fikira kutoziandika.

  • 7/23/2019 Poesia Swahili [Kezilahabi_Kithaka wa Mberia_Alamin Mazrui]

    20/20

    NiguseNitakapo kizuizini

    Nitamwomba yoyote mwendani

    aniguse

    taratibu

    polepole

    lakini

    kwa yakini!

    Niguse tena

    Unijuze tena

    Unifunze tena

    maisha yalivyo

    maisha yaonjavyo

    ladha yake ilivyo

    Nipo hapa nimekukabili

    Niguse tena tafadhali!

    Niguse!

    Niguse!

    UNFO

    Lanciato il 9/1/2016